JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA


 

 

BODI YA WAKURUGENZI WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

 

                                                                                                                                                                (Brigedia Jenerali Mstaafu, Yohana Ocholla Mabongo)

                                                                         (Mwenyekiti wa Bodi)

 

Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Ocholla Mabongo ni afisa jenerali mwanajeshi mstaafu aliyezaliwa tarehe 10 Novemba 1958 Butimba Mkoani Mwanza. Yeye ni mzaliwa wa pili kati ya wana wanne na binti watatu wa Bw Richard Ocholla Mabongo na Lydia Miko Gorio. Alisoma Shule ya Msingi Masonga Wilayani Rorya hadi mwaka 1974 alipojiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora kuanzia mwaka 1975 hadi Februari 1981 na kumaliza masomo yake ya kidato cha sita.

 

Juni 1981 kwa mujibu wa sheria alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa Ruvu JKT na miezi sita baadaye aliandikishwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Januari 1982. Mara tu baada ya kuajiunga na Jeshi, Februari 1982 alichaguliwa kuendelea na kozi ya uhandisi katika Chuo cha Ufundi cha Kijeshi huko Cairo Misri, na kuhitimu mwaka 1986 katika Shahada ya Kwanza ya Uhandisi (B.Sc. Engineering).

 

Mwaka 1987 Brigedia Jenerali mstaafu Yohana alijiunga na kozi ya Maafisa Wanafunzi katika Chuo cha Jeshi la Tanzania (Tanzania Military Academy) na kutunukiwa cheo cha Luteni Usu, na punde tu siku hiyo hiyo Luteni na kupelekwa katika Kikosi cha Jeshi la Anga kama Mkuu wa Patuni na kushika nyadhifa mbalimbali kama Mhandisi wa Mawasiliano wa Kikosi, Afisa Mawasiliano wa Kikosi, na Mkufunzi katika shule ya Kikosi. Kufuatia kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Mawasiliano ya Kijeshi na Chuo cha Anga cha Kijeshi na kufaulu vizuri Brigedia Jenerali alipandishwa cheo na kuwa Meja na kupewa uhamisho kwenda Chuo cha Mawasiliano ya Kijeshi mnamo mwaka 2001 kuwa Mkufunzi na Msaidizi Mkufunzi Mkuu.

 

Mnamo Oktoba 2001 Brigedia Jenerali Mstaafu Mabongo alihudhuria kozi ya Ukamanda na Unadhimu na baada ya kuhitimu 2002 alifanya kazi kama Afisa Mnadhimu wa Mawasiliano katika Makao Makuu ya Jeshi la Ulinzi  na baadaye mwaka huo huo 2002 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa Mwajiri Mkuu (Personal Assistant) hadi 2006 alipopandishwa cheo kuwa Luteni Kanali na mwaka mmoja baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kikosi katika Kikosi cha Mawasilianio (191) Wilaya ya Kisarawe hadi Oktoba 2008. Alipopandishwa cheo kuwa Kanali.

 

Mwaka 2008 baada ya kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Brig Jenerali mstaafu Mabongo alipandishwa cheo kuwa Kanali na kuteuliwa kuwa Afisa Mnadhimu Mawasiliano, Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu hadi 2015 alipopandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali, na Februari 2016 aliteuliwa kuwa Katibu wa Chuo katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi. Alihudumu kwa wadhifa huo hadi Julai 26, 2017 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, nafasi aliyoishikilia hadi alipostaafu tarehe 30 Juni 2018.

 

Brigedia Jenerali Mstaafu Mabongo, ni mhandisi aliyesajiliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Mwanachama wa Chama cha Wahandisi Tanzania (MIET). Pia ana Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Umeme kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1996) na Mafunzo ya Usalama kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (2014).

 

Brigedia Jenerali mstaafu amefanya safari nyingi za kimafunzo akiwa mwanafunzi na Mkufunzi katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi katika nchi mbalimbali zikiwemo; Afrika Kusini, Namibia, Botswana, Ethiopia, Zambia, Bangladesh, India, China, Vietnam, Denmark na Sweden. Safari hizi za kimafunzo zimempa fursa ya kuwa na uzoefu na ufahamu wa kutosha kwa kutaja machache katika nyanja za uongozi na utawala, usalama na mafunzo ya kimkakati, uhusiano wa kimataifa itifaki, na diplomasia. Tuzo alizowahi kupata ni pamoja na Medali Iliyotukuka, Medali ya Utumishi wa Muda Mrefu, Medali ya Kagera, Medali ya Miaka 40 ya Jeshi na Medali ya Miaka 20 ya Jeshi.

 

 

 

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA 2023