JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA


1. UTANGULIZI ( HISTORIA YA  POSTA NCHINI TANZANIA)

Kihistoria asili ya mawasiliano duniani yalianzia katika mfumo wa kiposta, ambapo watu na jamii mbalimbali ziliwasiliana kwa njia ya maneno ya mdomo au kwa maandishi kwa kutumia matarishi, punda, ngamia, wapanda farasi au watembea kwa miguu. Hawa walipokezana taarifa katika vituo vilivyoteuliwa kwenye njia kuu. Katika baadhi ya jamii za Kiafrika ikiwemo Tanzania, ngoma pia zilitumika katika kupeana taarifa. Mfumo huu uliwanufaisha zaidi wafalme na watawala wa kijadi ambao dhamira yao kuu ilikuwa kuwarahisishia uendeshaji wa shughuli za kiutawala hususan katika kuhakisha kuwa maelekezo, amri na miongozo yao inawafikia watawaliwa.

 

Mfumo huu ulikuwa ukiboreshwa sanjari na historia ya maendeleo ya binadamu na hadi kufikia karne ya kumi na nane huduma za Posta zikawa zinasimamiwa katika mifumo ya kitaasisi katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Mwaka 1874 ulianzishwa Umoja wa Posta Duniani (UPU) Umoja huu ambao makao yake makuu yako Mjini Berne - Uswizi ikiwa ni taasisi ya pili ya kimataifa kuanzishwa baada ya Umoja wa Mawasiliano ya Simu (ITU) mwaka 1865. UPU ni Shirika tanzu la Umoja wa Mataifa (UN) lenye jukumu la kusimamia maendeleo ya shughuli za Posta Kimataifa.

2.0  HISTORIA YA POSTA KABLA YA UHURU WA TANGANYIKA

Huduma za Posta kama taasisi zilianzishwa nchini na Serikali ya kikoloni ya Ujerumani ambayo ilitawala kwa pamoja nchi za Tanganyika, Rwanda na Burundi.

Makao Makuu ya Posta kwa nchi zote hizi yakiwa katika jengo la Posta ya Sokoine (Posta ya Zamani) jijini Dar es Salaam. Huduma ya kwanza ya barua iliyobandikwa stempu ilianzishwa hapa nchini mwaka 1893. Barua hizo zilitumwa kwa kutumia matarishi waliokuwa wanatembea kwa miguu umbali mrefu kutoka Makao Makuu ya Wilaya hadi Majimbo. Huduma ya treni kati ya Dar es Salaam hadi Kigoma na baadae hadi Mwanza na Arusha iliboresha mtandao wa huduma za Posta nchini.

Jengo la Posta ya Sokoine, Maarufu kama Posta ya Zamani, lililokuwa Makao Makuu ya Huduma za Posta kwa nchi za Tanganyika, Rwanda na Burundi, ambapo ni kitovu cha historia ya Posta Tanzania.

            2.1 MIUNDOMBINU YA OFISI ZA POSTA WAKATI WA WAKOLONI

Ofisi za Posta zilitengewa sehemu maalumu katika majengo ya utawala wa kikoloni (Boma) ikiwa ni pamoja na Bagamoyo, Kilimatinde, Biharamulo, Mahenge, Utete na Kilwa. Baadae, Utawala wa kikoloni wa Uingereza uliunda Idara ya Huduma za Posta chini ya Mkurugenzi wa Posta. Ilipofika mwaka 1925 Serikali ya Mkoloni wa Kiingereza ilianzisha Benki ya Akiba ya Posta Tanganyika baada ya kupitishwa Sheria ya Benki ya Posta ya Akiba ya Tanganyika na kuwekwa chini ya Mkurugenzi wa Posta kwa niaba ya Serikali Kuu ya Kikoloni.

             2.2 KUUNDWA KWA TAASISI YA HUDUMA AFRIKA MASHARIKI (EACSO)

Mwaka 1951 utawala huo uliunda chombo cha kusimamia huduma za pamoja katika nchi za Tanganyika, Kenya na Uganda yaani East African Common Services Organisation (EACSO). Aidha, chini ya Umoja huo ilitungwa sheria ya kuanzishwa Taasisi ya Posta na Simu ya Afrika Mashariki (EAP&TA) ambayo iliendelea kusimamia huduma hizi hadi wakati wa Jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1967.

  1. 3.0 HISTORIA YA POSTA KATIKA HARAKATI ZA UHURU

Katika kuimarisha nguvu za Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) chini ya Mwalimu Julius Nyerere na Chama cha Wafanyakazi cha Tanganyika Federation of Labour (TFL) chini ya Bwana Rashid Mfaume Kawawa, wafanyakazi wazalendo wa Posta walikuwa na Chama chao cha “National Union of Posts and Telecoms Employees (NUPTE). Makao Makuu ya Chama yalikuwa Dar es Salaam na kilikuwa na matawi katika ofisi zote za Posta nchini Tanganyika.  Hadi wakati wa Uhuru Mwenyekiti wa Chama hicho alikuwa ni Bwana Kweyamba na Katibu Mkuu Bwana Jacob Namfua ambaye baada ya uhuru aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa na Waziri. Malengo makuu ya NUPTE yalikuwa ni kutetea maslahi ya wafanyakazi wa Posta, lakini zaidi kuimarisha nguvu za TANU na TFL katika kudai uhuru ili kuondokana na sera ya ubaguzi iliyomweka mfanyakazi wa Kizungu juu, akifuatiwa na Muasia na Mzalendo akiwa chini kimaslahi kama mishahara na marupurupu.

 

  1. 4. 0 HISTORIA YA POSTA BAADA YA UHURU

Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Desemba 1961, huduma za Posta ziliendelea kusimamiwa chini ya Sheria iliyoanzisha Taasisi ya EAP&TA.  Pamoja na mambo mengine Taasisi hii ndiyo iliyokuwa na mamlaka pekee ya kusimamia kanuni na taratibu katika huduma za posta kwa nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika EAP&TA iliendelea kuwa chini ya Bodi iliyokuwa inaundwa na wajumbe wa nchi zote tatu za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Afisa Mtendaji aliendelea kuwa Postamasta Mkuu (Postmaster General), ambapo chini yake walikuwako Wakurugenzi wa ‘Mikoa’ ya kiposta (Regional Directors) wa nchi za Kenya, Uganda na Tanganyika. Makao makuu yaliendelea kuwa Nairobi nchini Kenya ambapo ofisi kuu ya “mkoa” wa Tanganyika ilikuwa ni Dar es Salaam, katika jengo la Posta ya Sokoine (Posta ya zamani).

5.0 UONGOZI WA POSTA BAADA YA UHURU

Menejimenti ya Makao Makuu ilisimamiwa na Mkurugenzi wa Mkoa na chini yake walikuweko wadhibiti wa Posta (Postal Controllers) wa Kanda mbili za Mashariki na Magharibi ambapo chini yao walikuweko “Assistant Postal Controllers”.  Katika ngazi ya mikoa ya kiserikali ilisimamiwa na Mapostamasta Viongozi (Head Postmasters).  Uongozi wote huu wa ngazi ya juu ulishikiliwa na raia wa kigeni hususan wazungu na wahindi.

6.0 JITIHADA ZA KURUDISHA UONGOZI WA POSTA KWA WANANCHI WAZAWA WEUSI WA AFRIKA MASHARIKI

Mara baada ya Uhuru zilianza jitihada za makusudi za kuhakikisha kuwa Taasisi ya EAP&TA inaongozwa na wazalendo kwani ilishadhihirika wazi kuwa Kenya na Uganda nazo zitapata uhuru karibuni. Sera hiyo ya kuwaandaa wazalendo ilifahamika kama “Africanisation”. Hata hivyo wazalendo wenyewe walipendelea kuiita sera hiyo ‘Naizesheni ili kuondoa dhana ya ubaguzi itokanayo na “Africanisation”. Baadae ili kuondoa mkanganyiko wa mitizamo ya kibaguzi kati ya wazalendo na wakoloni, sera hiyo ilianishwa na kuitwa “Localisation”                                                                        

Kwa upande wa Tanzania Bara viongozi wazalendo walioteuliwa kushika uongozi katika Ofisi za kanda ni pamoja na Bwana Rajabu Mabula Yusuf, Bwana Joseph Mhizi Lukindo na Bwana  P. S. Athuman.  Kwa mara ya kwanza katika historia, mwaka 1962 waliteuliwa wazalendo wachache kwenda nje ya nchi (Uingereza) kusomea uongozi wa ngazi ya juu katika shughuli za Posta (Senior Postal Management Course).  

                                                                      

              Bwana Rajabu Mabula Yusuf                                                      Bwana Joseph Mhizi Lukindo

 

Changamoto kubwa iliyokuwepo wakati huo ilikuwa ni kuhakikisha kuwa nafasi zote za uongozi zilizokuwa zimeshikwa na wageni zinashikiliwa na wazawa haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, ilipitishwa sera ya kuteua “mtu kwa mtu” (supernumerary appointment) ambapo wageni waliokuwa wameshika nafasi hizo za uongozi walilazimishwa kuendesha mafunzo kazini (on job training) kwa wazawa ili baada ya muda uliopangwa, nafasi zote zishikiliwe na wazawa. Chini ya sera hii, mgeni ambaye angeshindwa kufundisha mzawa ili achukue nafasi yake, angechukuliwa hatua kali za kinidhamu.

 

7.0 POSTA NA JUMUIYA YA AWALI YA AFRIKA MASHARIKI (EAC)

 Mara ya baada ya nchi zote za Kenya, Uganda na Tanzania kupata uhuru ilianzishwa Jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki. (EAC). Kuanzishwa kwa Jumuiya hii tarehe 1 Desemba 1967, kulilenga “katika kuimarisha na kusimamia mahusiano ya kibiashara na uchumi wa nchi wanachama na kuhakikisha kuwa kuna uwiano sawa wa maendeleo  yatokanayo na ushirikiano huu”.  Chini ya sheria iliyoanzisha Jumuiya hiyo lilikuwepo Bunge la Afrika Mashariki ambalo jukumu lake kubwa lilikuwa ni kutunga sheria za kusimamia maeneo muhimu ya ushirikiano ikiwa ni pamoja na huduma za Posta.

8.0 SHIRIKA LA POSTA NA SIMU LA AFRIKA MASHARIKI (EAP&TC)

Kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki (EAP&TC), Shirika hilo liliwajibika kuendesha shughuli zake kibiashara katika nchi zote za Jumuiya hiyo.  Hata hivyo kutokana na unyeti wa huduma za Posta, Shirika hilo liliwajibika pia kuhakikisha kuwa huduma hizo hususan zile za msingi kama za utumaji wa barua, vifurushi, vipeto na fedha zinawafikia watu wengi zaidi wa mijini na vijijini.   Mantiki ya kuweka umuhimu wa huduma za msingi za Posta ilizingatia ukweli kuwa huduma hizo ndizo pekee zilizowafikia wananchi wengi na kwa gharama nafuu.

 9.0 WATANZANIA VIONGOZI WAKUU (EAP&TC)

Kutokana na uendeshaji wa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki kila nchi iliwajibika kutoa Postamasta Mkuu ambapo Mnamo mwaka 1964 Postamasta Mkuu Mwafrika wa kwanza alikuwa ni Mtanzania Bwana John Ketto ambaye alikuwa wa kwanza kuongoza chombo hiki baada ya kustaafu kwa Postamasta Mkuu aliyekuwa Raia wa Kigeni Bwana Ivers. Postamasta Mkuu huyu aliteuliwa na Mamlaka ya Marais watatu wa Afrika ya Mashariki kushika nafasi hiyo.  Baada ya kuanzishwa kwa Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki Bwana John Ketto aliendelea kuwa mtendaji Mkuu wa Shirika hilo lakini kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu.  Makao Makuu ya Posta na Simu yaliyokuwa Nairobi nchini Kenya, na baadae yalihamia Kampala nchini Uganda mwaka 1967.

 

Baada ya Bwana John Ketto kumaliza kipindi chake, Mtanzania mwingine Bwana Rajabu Mabula Yusuf aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hili kuanzia mwaka 1976. Kabla ya hapo Bwana Rajabu Yusuf alikuwa ni Mkurugenzi wa Mkoa wa Tanzania.  Baada ya hapo nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Mkoa wa Tanzania ilishikiliwa na aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia shughuli za Posta Bwana Raymond Mzuguno. (Kipindi hicho Nchi zilikuwa zikitambuliwa kama mikoa ya kiposta ambapo makao Makuu yakiwa Nchni Uganda)

                       

               Bwana Raymond Mzuguno.

10. UPANUZI WA MIUNDOMBINU YA POSTA WAKATI WA JUMUIYA

Ofisi nyingi za Posta za Wilaya na Mikoa zilijengwa wakati wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa lengo la kuhakikisha kuwa ofisi hizi zinakuwa Posta kamili zinazotoa huduma zote za Posta, ikiwa ni pamoja na huduma za uwakala za Benki ya Posta.  Katika mpango huo yalijengwa Makao Makuu ya sasa ya Shirika la Posta – Posta House, Posta Kuu (GPO) ya Dar es Salaam, Posta kuu ya Zanzibar ya Kijangwani ambapo huko Pemba zilijengwa Posta za Chake Chake, Wete, Mkoani na Mkokoteni. 

       

Makao Makuu ya Shirika la Posta kwa upande wa Tanzania. (Picha ya 1994)

 

Ilikuwa ni kipindi hiki cha Jumuiya wakati kilipojengwa Chuo cha kwanza cha Posta Nchini kilichokuwa katika eneo la Shauri Moyo, Ilala iliko sasa Shule ya Sekondari ya Kislamu ya AL_HARAMAIN.  Baadae majengo ya Chuo hicho yalikabidhiwa kwa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na hivyo Chuo cha Posta na Simu kujengwa eneo la Kijitonyama pia jijini Dar es Salaam.  Chuo hiki sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

                                       

11. VITA YA TANZANIA NA UGANDA ILIVYOATHIRI MAKAO MAKUU YA POSTA NA SIMU YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI.

Nchini Uganda ndiko kulikokuwa Makao Makuu ya Shirika la Posta na Simu la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyofanywa na Iddi Amin Dada dhidi ya Rais Milton Obote wa Uganda, hali ya usalama nchini Uganda ilizorota sana kiasi cha kutishia Watanzania na Wakenya waliokuwa wakifanya kazi Kwenye Makao Makuu hayo Nchini Uganda. Kilikuwa ni kipindi kigumu mno katika uendeshaji wa shughuli za Posta katika nchi zote za Afrika Mashariki, kwani vikao vya kutoa maamuzi vilikuwa havifanyiki na ilitokea hali ya kutoaminiana miongoni mwa wafanyakazi wa Shirika hilo. Ilifikia hatua shughuli za Makao Makuu zikawa zinasimamiwa katika miji miwili ya Kampala na Nairobi. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 1976 baadhi ya raia wa kigeni wakiwemo watanzania walianza kutoroka nchini Uganda wakihofia usalama wao. Ilipofika mwezi Aprili mwaka 1977 shughuli zote za Shirika la Posta na Simu la Afrika Mashariki zikasimama rasmi na hivyo wafanyakzi wa Tanzania waliokuwa nchini Uganda na Kenya wakarejea nyumbani.

 

12. KUUNDWA KWA SHIRIKA LA POSTA NA SIMU TANZANIA (TP&TC)

Kutokana na kusambaratika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Serikali ya Tanzania iliteua kamati ya kuandaa sheria ya kuunda Shirika la Posta na Simu Tanzania ili kuchukua nafasi ya Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki. Shirika jipya liliundwa kwa Sheria ya Bunge Nambari 15 ya mwaka 1977 iliyoanza kutumika rasmi tarehe 3 Februari mwaka 1978. Muswada wa kutunga sheria hii uliwasilishwa Bungeni na Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi Ndugu Amir Jamal ambaye pia alisimamia huduma nyingine zilizojumuishwa chini ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kama Reli, Bandari, Ndege, Usalama wa Anga na Hali ya Hewa.

 

13. VIONGOZI WAANZILISHI WA SHIRIKA (TP&TC)

Baada ya kuanzishwa Shirika hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alimteuwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara mbalimbali Bwana Fredrick Mchauru kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kwanza na Bwana William Maeda ambaye alikuwa Katibu wa Kampuni ya Simu za Nje za Afrika Mashariki kuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Shirika la Posta na Simu Tanzania.  Idara ya huduma za Posta katika Shirika hili ilikuwa chini ya Mkurugenzi (Director of Postal Services-DPS) Bwana Francis Mark Chengula.

 

13.1 MAJUKUMU YALIYOKUWA YAKIFANYIKA NI PAMOJA NA:

  • Kuratibu na kusimamia mawasiliano yote ya Posta katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  • Kuhakikisha kuwa huduma za msingi za mawasiliano ya Posta hasa za barua na vifurushi zinawafikia watu wengi zaidi wa mijini na vijijini.
  • Kuweka mipango endelevu ya kuwezesha huduma za Posta zichangie maendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii.

 

14. HISTORIA YA MTANDAO WA EMS KATIKA TANZANIA

Kutokana na mageuzi ya kiuchumi yaliyoenda sambamba na mabadiliko ya mahitaji na vionjo ya wateja, ilipofikia mwaka 1985 kwa mara ya kwanza ilianzishwa huduma ya Expedited Mail service (EMS) nchini Tanzania.  Huduma hii ilianzishwa ikiwa na wateja wawili tu wa Dar es Salaam, ambao walikuwa wanapokea wastani wa barua nne tu kwa siku.  Huduma hii ilianzishwa kufuatia makubaliano kati ya Shirika la Posta la Uingereza (Royal Mail) na Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC).  Chini ya makubaliano hayo, huduma hiyo ilishughulikia barua za EMS zinazotoka Uingereza tu kuingia nchini (inbound) na kusambazwa katika jiji la Dar es Salaam tu.

 

Mwaka huo wa 1986 Shirika lilianzisha huduma hii ya EMS kwa nchi nyingine za Ulaya kama Ufaransa, Ubelgiji, Ugiriki, Uholanzi na Norway.  Hata hivyo, huduma ilikuwa ni ya kupokea barua na vifurushi vya kutoka katika nchi hizi (inbound) na sio kutoka Tanzania kwenda huko (out-bound). Ilipofikia mwezi Agosti mwaka 1987 Shirika kwa mara ya kwanza liliingia kwenye makubaliano na nchi nyingine zaidi zipatazo 22 za Ulaya Magharibi, Asia, Amerika na Mashariki ya Kati ya kushirikiana katika kupokea barua na vifurushi vya EMS vinavyoingia na kutoka nchini.

 

Aidha, kutokana na maendeleo ya teknolojia, mwaka 1993 Shirika lilianzisha huduma mpya za EMS MONEYFAX na EMS FAX hapa nchini Tanzania. Huduma hizi zitokanazo na teknolojia ya kielotroniki zilianzishwa kuzingatia mahitaji ya soko kwa wakati huo.

 

15. KUANZISHWA KWA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA (TPC) MWAKA 1994

15.1 HISTORIA YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

 Shirika la Posta Tanzania lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge No. 19 ya mwaka 1993 (Tanzania Posts Corporation Act. 1993) baada ya kurekebishwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC). Katika mabadiliko hayo Taasisi tatu ziliundwa yaani Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) kwa sasa ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL),Sasa Shirika la Mawasilisno Tanzania. Mabadiliko hayo yalilenga kuleta maboresho katika Sekta ya Mawasiliano ili sekta hiyo iwe kichocheo cha maendeleo ya Taifa.

Shirika la Posta lilianza kazi rasmi tarehe 1 Januari 1994. Shirika linamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100. Aidha Shirika liko chini ya Umoja wa Posta Duniani (UPU), Umoja wa Posta Afrika(PAPU), Umoja wa Posta Kusini mwa Afrika (SAPOA) na Taasisi ya Mawasiliano ya Afrika ya Mashariki(EACO).

 

Majukumu ya msingi ya Shirika yaliyotokana na Sheria hiyo ni pamoja na;

  1. Kutoa huduma za Posta ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
  2. Kutosheleza mahitaji ya kitaifa ya huduma za Posta za Viwanda, Biashara na jamii kwa ujumla ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
  3. Kutoa huduma za kutuma na kulipa fedha kwa njia ya hawala za Posta (Money Order, Postal Order) au kwa kutumia njia nyingine zinazoonekana zinafaa ndani na nje ya nchi;
  4. Kutoa huduma za kaunta kwa ajili ya jamii na Serikali kulingana na malengo yaliyotajwa katika sheria ya uanzishwaji wa Shirika

 

15.2 VIONGOZI WA SHIRKA LA POSTA

Viongozi waaanzilishi wa Shirika ni Profesa Geofrey Mmari aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Wakurugenzi na Bwana Sulemani Msofe aliyekuwa Postamasta Mkuu wa kwanza.

Wenyeviti wa Bodi waliofuatia ni Bwana David Wakati (1996 – 2004)  Bwana Yona  Killagane (2004 – 2008), Dkt. Yamungu Kayandabila (2008-2016), Kanali Mstaafu Dkt. Haruni Kondo (2017-2021) na aliyepo sasa ni Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Ocholla Mabongo (2022- hadi sasa )

Mapostamasta Wakuu ni Bwana Lucian Benedict Minde (2001 – 2007), Bwana Deos Khamisi Mndeme (2007 – 2015), Bwana Fortunatus Furtunis Kapinga alikaimu nafasi ya Postamasta Mkuu (2015- 2017) alipostaafu baada ya hapo aliteuliwa kukaimu nafasi ya Postamasta Mkuu Bwana Deogratias Charles Kwiyukwa (Machi – Novemba 2017), Bwana Hassan Abeid Mwang’ombe (2017-2021), Bwana Macrice Daniel Mbodo (2021- 2023), Maharage Ally Chande - (2023- Sasa).

 

PICHA ZA WENYEVITI WA BODI YA WAKURUGENZI TANGU MWAKA 1994- 2022

                

Prof.Jofrey Mmary -Mwenyekiti wa Kwanza wa Bodi ya Wakurugezi wa Shirika la Posta Tanzania (1994- 1996)

       

 

Bw. David wakati- Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugezi wa Shirika la Posta Tanzania (1996- 2004)

 

           

 

Dkt. Yamungu Kayandabila -Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugezi wa Shirika la Posta Tanzania (2008- 2014)

 

Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo -Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugezi wa Shirika la Posta Tanzania (2017-2021)

 

 Brigedia Jenerali Mstaafu, Yohana Ocholla Mabongo- Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugezi wa Shirika la Posta Tanzania (2022- Sasa)

 

PICHA ZA MAPOSTAMASTA WAKUU TANGU MWAKA 1994- 2022

Bw.Suleiman Msofe- Postamasta Mkuu (1994-2001)

 

Bw. Lucian B.Minde -Postamasta Mkuu (2001- 2007.)

 

Deos Kh. Mndeme- Postamasta Mkuu (2008- 2015)

 

Fortunatus F. Kapinga -Kaimu Postamasta Mkuu (2015- 2017)

 

Deogratius C. Kwiyuka -Kaimu Postamasta Mkuu (Machi-Novemba, 2017)

 

 

Hassan A. Mwang’ombe- Postamasta Mkuu (2017- 2021)

 

Macrice D. Mbodo - Postamasta Mkuu (2021-  2023)

 

Maharage Ally Chande - Postamasta Mkuu (2023- Sasa)

 

Makao Makuu ya Shirika la Posta (2022)

….……………MWISHO ……………………

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA