BODI YA WAKURUGENZI WA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA YAZINDULIWA.

25 March 2020

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, akimkabidhi nyundo pamoja na vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania (TPC), Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo (kushoto), alipokuwa akiizindua Bodi hiyo, jijini Dar es Salaam leo.

 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amezindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) jijini Dar es salaam. Katika uzinduzi huo uliofanyika tarehe 2 Februari 2020, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alizindua Bodi hiyo kwa kumkabidhi nyundo pamoja na vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi mpya ya Shirika la Posta Tanzania (TPC), Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo.

Mheshimiwa Kamwelwe alielezea imani yake kwa bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake Dr.Haruni Kondo, kuwa itaimarisha usimamizi katika utekelezaji wa mikakati na malengo mbali mbali ili kuboresha utendaji wa TPC na hivyo kuliwezesha kuchangia katika maendeleo ya taifa letu. Uzinduzi wa bodi hiyo umefuata baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kumteua Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo kuendelea kuwa Mwenyekiti wa bodi hiyo kwa awamu ya pili baada ya kipindi cha awali cha miama mitatu kumaliza.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano (Mawasiliano), Kitolina Kippa aliwatambulisha wajumbe wa bodi hiyo, ambao ni Dkt. Ubena Agatho John, Bi. Fatma Bakari Juma, Mhandisi Augustine Matthew Mbalamwezi, Erick Francis Shitindi, Bwire Magere na Michael Masinda ambao uteuzi wao ni wa kipindi cha miaka mitatu kuanzia tarehe 20 Januari, 2020.

Mwenyekiti wa bodi ya TPC, Kanali Mstaafu, Dkt. Haruni Kondo amesema kuwa Bodi hiyo ipo tayari kuendesha TPC sambamba na spidi ya Mhe.Rais, kwa kuwa ina wajumbe wazalendo na wako  tayari kufanya kazi zaidi ili kuongeza faida, kusimamia rasilimali za Shirika kwa maendeleo ya taifa letu.

Nae Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bwana, Hassan Mwang’ombe akisoma taarifa ya utekelezaji wa Shirika, na kusema kuwa Shirika linatumia shilingi milioni 69 hadi 75 kwa mwezi kulipa pensheni kwa wastaafu wa iliyokuwa Shirika la Posta na Simu la iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo alielezea kua Shirika la Posta sio mfuko wa hifadhi ya jamii.

Bwana Mwang’ombe ameiomba bodi mpya kwa kushirikiana na Serikali kusaidia TPC kupata mtaji wa kuendesha Shirika hilo kwa faida ili waweze kuendelea kutoa gawio zaidi.

Pia Uzinduzi huo ulihudhuriwa na baadhi ya wajumbe kutoka wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania, na Waandishi wa habari.

Imetolewa na:

Kitengo cha habari

Shirika la Posta Tanzania,

Makao Makuu, Dar es Salaam

Top
X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!