DKT. ZAINABU CHAULA, KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO ATEMBELEA NA KUKAGUA UJENZI WA JENGO LA UMOJA WA POSTA AFRIKA.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Dkt. Zainabu Chaula, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Jijini Arusha Tarehe 21 Juni 2020. 
 
Ujenzi huo unafanywa kwa ubia baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na PAPU kwa gharama ya shilingi bilioni 33.58 mpaka kukamilika kwake, ambapo unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni 2022.
 
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Chaula ameridhika na maendeleo ya ujenzi huo na kutoa wito kwa wananchi kuzidi kuiamini Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kufanya vizuri, kwani kwa kupitia ujenzi huo nchi itanufaika kwa mikutano na vikao vya kimataifa hivyo kuingiza fedha za kigeni na kutoa ajira za moja kwa moja kwa wananchi ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa na malighafi zinazotumika katika ujenzi huo zinapatikana nchini.
 
 
Jengo hilo linamilikiwa na Serikali kupitia TCRA kwa asilimia 40 na PAPU asilimia 60 ambazo ni michango ya nchi 45 wanachama wa PAPU ambapo Tanzania ni nchi mwanachama na inachangia dola za marekani 33,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 75 kwa mwaka.
 
 
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Mawasiliano, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo utaleta mandhari mpya ndani ya jiji la Arusha na kutupa fahari kama nchi kuweza kutunza na kuifadhi taasisi za kimataifa nchini.
 
“Sisi kama Sekta ya Mawasiliano tutahakikisha jengo hili linakamilika kwa muda uliopangwa kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi na kwa kiwango cha kimataifa ili kuonesha uwezo wa nchi kujenga majengo yenye hadhi ya kimataifa”, alisema Dkt. Yonazi.
 
 
Imetolewa na Kitengo cha Uhusiano
Shirika la Posta Tanzania
 
Top
X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!