TAARIFA YA ZIARA YA KATIBU MKUU WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MAWASILIANO) ALIPOTEMBELEA MAKAO MAKUU YA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA.

 Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano) Mheshimiwa Dkt. Zainabu Chaula amelitaka Shirika la Posta Tanzania kuongeza kasi ya uzalishaji kwa kutoa huduma bora zinazoendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

Dkt. Chaula aliyasema hayo tarehe 24 Agosti, 2020 wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kwanza ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania tangu ateuliwe kushika wadhifa wa Katibu Mkuu (Mawasiliano) tarehe 22 Aprili, 2020 ikilenga kujionea shughuli mbalimbali zinayofanywa na Shirika la Posta Tanzania.

Katibu Mkuu alipata pia wasaa wa kuzungumza na wafanyakazi wa Shirika la Posta na kuwaasa kuacha kufanya kazi kwa mazoea, bali wafanye kazi kwa tija, nidhamu, bidii kwa ajili ya matokeo mazuri ya Shirika na maslahi mapana ya Taifa. 

“Ni vyema kila mtu akawajibika kwa nafasi yake, akiheshimu kila mtu, kuwa na upendo, bidii, nidhamu ya kazi na kuuheshimu uongozi kwa matokeo makubwa ya Shirika”. Alisema Dkt. Chaula.  

Aidha, Dkt Chaula alitembelea ukarabati wa Jengo la Posta kuu ya Dar es Salaam (GPO), ambao unalenga kuifanya Posta kuwa sehemu za kisasa za kutolea huduma, huku akisisitiza usimamizi mzuri kwa wakandarasi ili waweze kufanya kazi yenye thamani ya fedha “value for money”.

Dkt. Chaula aliongezea kuwa, Changamoto zilizo nyingi hutokana na kutokuwajibika kwa wasimamizi na hivyo amemtaka Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Dkt. Haruni Kondo kuendelea kusimamia kwa ukaribu utendaji wa Shirika kwa nia ya kuongeza mapato hata kufanikisha kutoa gawio linalostahili kwa Serikali kulingana na rasilimali zilizowekezwa ndani ya Shirika la Posta.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Dkt. Haruni Kondo alimshukuru Dkt. Zainab Chaula kwa kuja kulitembelea Shirika na kuipongeza Menejimenti ya Shirika hilo, wafanyakazi na watendaji wote kwa bidii na uzalendo wao katika kuhakikisha Shirika linaendelea kutoa huduma zake vizuri kama inavyotakiwa.

Dkt. Kondo aliongezea kuwa, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania inaendelea kutimiza wajibu wake wa kulisimamia Shirika ili liendelee kutoa huduma bora na kwa gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

“Bodi hii inaangalia sehemu mbili haki na wajibu, tushirikiane kudhibiti hawa wasiotaka kuwajibika, kwa sababu hii ni vita yetu wote, Bodi haiwezi kufanya kazi peke yake pasipo ushirikiano wenu”. Alisisitiza.

Hata hivyo, kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Daniel Mbodo alihitimisha kwa kusema kuwa, amefurahishwa na ujio wa Katibu Mkuu Dkt. Zainab Chaula na kuahidi kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa ili kuongeza uzalishaji na mapato ya Shirika kwa maendeleo ya Taifa letu. 

 

Imetolewa na ofisi ya Mawasiliano

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Top
X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!