UJUMBE WA POSTAMASTA MKUU, SIKU YA POSTA DUNIANI.

Tarehe 9 Oktoba, 2020, Shirika la Posta Tanzania (TPC) linaungana na wadau wengine wa Posta duniani kote kuadhimisha miaka 146 ya Umoja wa Posta Duniani (UPU).

Kauli mbiu ya mwaka huu Posta "NI ZAIDI YA BARUA" huku Ulimwengu mzima ukiwa unapitia kipindi cha janga la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya Corona.

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, kwa niaba ya Menejimenti ya Shirika na kwa niaba yangu mimi binafsi, ningependa kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani, Balozi Bishar Hussein kwa maadhimisho ya mwaka huu, huku tukishuhudia safari ya mafanikio ya Sekta ya Posta Duniani kwa miaka 146.

Kihistoria Shirika hilo lilianzishwa Mwaka 1874, likiwa na makao yake makuu mjini Berne, Uswisi. Shirika hili ni kati ya Mashirika makongwe zaidi duniani na likichukua nafasi ya pili kwa ukongwe ulimwenguni. Balozi Bishar akiwa

Mkurugenzi Mkuu wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa mtandao wa Posta Duniani unatumikia ipasavyo na kuhudumia maisha ya watu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi hata katika nyakati ngumu.

Tunapoingalia kauli mbiu ya mwaka huu,”NI ZAIDI YA BARUA” inaadhimishwa duniani kote hata katika kipindi hiki cha janga la KORONA, pamoja na magumu hayo Posta imesimama imara kufanya kazi zake bila uoga kuwahudumia wananchi.

Kama sote tunavyoelewa, jukumu la Posta sio tu kutuma barua na vifurushi pekee bali pia kutoa ufumbuzi wa usafirishaji wa taarifa muhimu na uunganishaji wa mtirirko wa takwimu muhimu, pia utumaji wa taarifa na kufanya miamala ya kifedha kote ulimwenguni.

Tunapotazama nyuma na kufuatilia tunaridhishwa na historia ya mabadiliko katika Sekta Posta, mtagundua kuwa juhudi zilizofanyika na Umoja huu zimewezesha sekta ya Posta kusimama imara katika soko na kuhudumia mpaka  leo. Ukweli ni kwamba Posta ndio mtandao wa zamani zaidi wa mawasiliano, ambayo bado una jukumu muhimu katika utoaji taarifa na utumaji wa bidhaa Duniani.

Posta imefanikiwa kutumia changamoto za maendeleo ya kiteknolojia kama fursa kwa namna mbalimbali na kujitangaza pia kubuni mbinu mpya za kimasoko na biashara ambazo ndizo zinazofanya Posta ionekane ni zaidi ya utumaji wa barua.

Kwa mfano, wakati wa janga la ugonjwa wa COVD-19 nchini Tanzania,Shirika la Posta lilitumia vizuri mtandao wake mpana tulionao nchini kote na hata ule matumizi ya TEHAMA ulioanzishwa kwa dharura kutumikia jamii kwa kupeleka vifaa kinga vya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona na huduma za kifedha kwa jamii. Mfumo TEHAMA uliuwanganisha wafanyikazi wetu wa operesheni ambao walifanya kazi usiku na mchana kupeleka sampuli za damu kwa maabara zilizokusudiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Aidha, Shirika limeendelea kutumia mtandao wake mkubwa na wa kuaminika kuwezesha wanafunzi wa elimu ya juu kupeleka fomu zao za maombi ya mikopo  kwenye ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu jijini Dar es Salaam, kulipa pensheni za wastaafu kwa niaba ya kampuni za pensheni na pia kutoa huduma ya nyaraka za Mahakama kwa wakati kwenye jamii popote walipo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika eneo la kifedha, tuna ushahidi kuwa Shirika lina ushirikiano wa kibiashara na benki nne za ndani ambazo ni benki ya NMB, NBC , benki ya CRDB na Benki ya Watu ya Zanzibar(PBZ) ili kutoa huduma za kifedha mahali ambapo jamii ina uhitaji wa huduma hiyo nchini kote. Haya ni kati ya mambo yanayodhihirisha kuwa Posta ni zaidi ya barua.

Katika eneo la biashara Mtandao, Shirika lina maduka mawili ya kimtandao ambayo moja linashughulika na uuzwaji wa stempu za mtandaoni huku la pili likishughulika na uuzwaji wa bidhaa mbalimbali. Duka hili la Mtandao linawezesha wafanyabiashara wadogo na wakati kujitangaza ulimwengu kote na kukuza biashara zao kupitia duka la Posta la mtandao almaarufu kama “Posta online shop”. Hivyo hii inathibitisha kuwa Posta ni zaidi ya barua.

Ukiangalia Umoja wa Posta Duniani kwa sasa, umeweza kujijengea mtandao mpana wenye wanachama nchi 192 zilizo na ofisi za posta kamili zaidi ya 660,000. Tunatoa wito kwa wahusika wote muhimu katika sekta ya posta kama Forodha na wasafirishaji kuzingatia mtandao huu na kuutumia kikamilifu ili kuwahudumia wananchi wetu kuwawezesha kufanya biashara mtambuka. Sisi kama Shirika tuko katika kufanya kazi kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika kuhudumia jamii yetu.

Leo tunapoadhimisha miaka 146 ya Umoja wa Posta Duniani, tunawashukuru wadau wetu wote haswa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia  Wizara yetu ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kutuwekea mazingira wezeshi hii imetuwezesha kuhudumia wateja wetu na kuendelea kutimiza majukumu yetu ya kutoa huduma za ubunifu na zinazowafikia wateja kwa urahisi.

Tunapoadhimisha siku hii muhimu tunapenda kuwahakikishia kuwa Shirika la Posta lina dhamira ya dhati ya kuitumikia jamii na kuwadhibitishia kuwa Posta si utumaji wa barua pekee, bali ni jukwaa muhimu la kuchangia juhudi za Serikali katika kukuza uchumi. Aidha Shirika hili litabaki kuwa bora katika ubunifu na utoaji huduma zenye kukidhi mahitaji ya wateja wetu kwa wakati.

"Posta ni zaidi ya barua"

 

HASSAN MWANG’OMBE

POSTAMASTA MKUU

Top
X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!