BURIANI DKT JOHN POMBE MAGUFULI

 

Shirika la Posta Tanzania(TPC) linatoa pole za dhati kwa Watanzania wote kufuatia kifo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Dkt. John Pombe Magufuli, alikuwa ni Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2015 mpaka mauti ilipomfika. Katika uongozi wake Dkt. Magufuli atakumbukwa kwa uchapakazi wake mahiri, Kuzuia mianya ya rushwa na kusimamia utekelezaji wa maendeleo ya Taifa.

Hakika Taifa limepoteza kiongozi shupavu, mahiri, Mcha Mungu na mzalendo wa kweli. Shirika la Posta linaungana na Watanzania wote kuomboleza msiba huu mzito wa kitaifa.


UFUATAO NI WASIFU WA HAYATI DKT. JOHN POMBE MAGUFULI,


KUZALIWA

Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa Oktoba 29 mwaka 1959 huko Chato mkoani Geita, Kaskazini magharibi mwa Tanzania.

ELIMU

Dkt. John Magufuli alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Chato kuanzia mwaka 1967 hadi 1974. Mwaka 1975 alijiunga na Seminary ya Katoke iliyo Biharamulo, Kagera kwa elimu ya Sekondari na kisha kujiunga na shule ya sekondari ya Lake iliyoko Mwanza hadi 1978 alipohitimu. Mwaka 1979 alijiunga na shule ya Sekondari ya upili ya Mkwawa, Iringa kwa ajili ya masomo ya kidato cha tano na sita na kuhitimu Mwaka 1981.

Mwaka 1981 hadi 1982 alisomea Stashahada (Diploma) ya Ualimu wa masomo ya Sayansi katika Chuo cha ualimu cha Mkwawa, Iringa masomo makuu yakiwa Kemia na Hisabati. Akiwa kazini, Dkt. John Magufuli aliamua kujiendeleza kwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1985 hadi 1988 alipotunukiwa Shahada ya ualimu katika masomo ya Kemia na Hisabati.

Mwaka 1991 hadi 1994 alisomea Shahada ya Uzamili ya Kemia (Msc. Chemistry) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Tanzania na Chuo Kikuu cha Salford, Uingereza. Mwaka 2009 alitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

MAFUNZO YA KIJESHI

Kati ya Mwaka 1983 na 1984, Dkt. John Pombe Magufuli alipata mafunzo ya kijeshi kwa mujibu wa sheria kwenye Kambi za Jeshi la Kujenga Taifa Makutupora - Dodoma, Makuyuni - Arusha na Mpwapwa - Dodoma.

KAZI

Baada ya kufuzu Stashahada ya ualimu, alifundisha masomo ya Hisabati (Mathematics) na Kemia (Chemistry) katika shule ya Sekondari Sengerema kuanzia mwaka 1983. Baada ya hapo akafanya kazi kama Mkemia katika Chama cha Ushirika cha Nyanza huko Mwanza hadi mwaka 1995.

NAFASI ZA KISIASA

Mwaka 1995 Dkt. John Pombe Magufuli aliingia katika ulingo wa siasa pale alipoamua kugombea ubunge katika Jimbo la Chato na kushinda uchaguzi huo wa ubunge. Mwaka huo huo Dkt. Joh Pombe Magufuli aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin Wiliam Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyohudumu hadi Mwaka 2000.

Baada ya uchaguzi Mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyohudumu hadi Mwaka 2006 alipohamishwa kwenda Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi alipokaa hadi Mwaka 2008. Mwaka 2010, aliteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi kwa mara ya pili na kudumu kwenye nafasi hiyo hadi Mwaka 2015.

NAFASI YA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

Mnamo Tarehe 12 Julai 2015, Dkt. John Pombe Magufuli aliteuliwa kuwa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Akiwa na Mama Samia Suluhu Hassani kama mgombea mwenza.


Tarehe 29 Oktoba 2015 alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Rais wa Awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wa kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46%. Magufuli aliapishwa kama Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 5 Novemba 2015.

MUHULA WA PILI WA KIPINDI CHA URAIS

Mnamo tarehe 30 Oktoba 2020, Tume ya Uchaguzi Tanzania ilimtangaza Dkt. John Pombe Magufuli kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa muhula wa pili kwa kupata kura milioni 12.5 hiyo ikiwa ni sawa na asilimia 84.

Mpaka umauti unamfika tarehe 17 Machi 2021, Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shirika la Posta Tanzania linatoa pole kwa Watanzania wote na Mungu ailaze roho ya Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli Mahali pema Peponi.

BWANA AMETOA, BWANA AMETWAA, JINA LAKE LIHIMIDIWE!

Na Rachel Kitinya
OFISI YA MAWASILIANO
SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

 

0fb66196cff5498d8785a9fe8a93bfde

Top
X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!