📍POSTA TANZANIA YAPOKEA UGENI KUTOKA POSTA KENYA📍
POSTA TANZANIA YAPOKEA UGENI KUTOKA POSTA KENYA
Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo amepokea ujumbe kutoka Shirika la Posta Kenya. Ujumbe wa Posta ya Kenya umeongozwa na Postamasta Mkuu wa Shirika hilo Bw. Daniel Kagwe akiambatana na Maafisa waandamizi kutoka Shirika Hilo
Bw. Daniel Kagwe amekuja nchini Tanzania kwa lengo la kukuza mahusiano na mashirikiano ya kibiashara baina ya nchi hizi mbili kupitia mashirika haya hususani katika maeneo ya biashara mipakani mwa nchi hizi (Cross Border Business) hasa katika eneo la usafirishaji.
Katika ziara hiyo Bw.Daniel Kagwe akiongozwa na mwenyeji wake Bw. Macrice Mbodo alipata wasaa wa kutembelea Ofisi za Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU) yaliyopo jijini Arusha, ambapo Kenya pia ni nchi mwanachama wa Umoja huo
Aidha, akiwa katika Ofisi za PAPU Postamasta Mkuu wa Kenya Bw. Kagwe na Bwana Mbodo walipata nafasi ya kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja huo Bw. Sifundo Chief Moyo ambapo Kenya na Tanzania chini ya Umoja huo wameona iko haja ya kuendelea kukuza mahusiano kwani taasisi zote hizi zinategemeana.
Kikao hicho pia kilijadili namna ambavyo sekta ya Posta inaweza kuleta tija barani Afrika na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi na Afrika kwa ujumla kwa kutoa huduma bora na zenye tija na zinazoendana na mahitaji ya wananchi hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko na maendeleo ya Teknolojia
Sambamba na hilo, kikao hicho kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa PAPU Bw. Sifundo Moyo kilijadili namna ambavyo watendaji wa mashirika ya Posta barani Afrika wanapaswa kupatiwa mafunzo ya namna ya kufanya shughuli za uendeshaji katika mashirika haya ili kuongeza weledi katika utendaji wao
Katika hatua nyingine, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Kagwe akiambatana na mwenyeji wake Bw. Mbodo walitembelea na kujionea ujenzi unaoendelea wa jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika, jijini Arusha
Katika ziara hiyo, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe alitembelea ofisi za Shirika la Posta Mkoani Arusha na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika la Posta mkoani humo
Bw. Kagwe anatarajiwa kuendelea na ziara yake nchini Tanzania kwa kutembelea Makao Makuu ya nchi jijjni Dodoma na anatarajia kutembelea Wizara inayosimamia sekta ya Posta (Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari)
Ziara hiyo imejumuisha Maafisa waandamizi kutoka Shirika la Posta Tanzania pamoja na maafisa waandamizi kutoka Shirika la Posta Kenya
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano,
Shirika la Posta Tanzania,
13 Disemba, 2021
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe (wa pili kulia) akizungumza jambo na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta nchini Bw. Macrice Daniel Mbodo (kulia) wakati alipotembelea ofisi za Shirika la Posta nchini mkoani Arusha na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo mkoani humo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Bw. Sifundo Chief Moyo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe (kulia) na Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Daniel Mbodo (kushoto) mara baada ya kikao chao, jijini Arusha
Viongozi waandamizi kutoka Shirika la Posta Tanzania, Shirika la Posta Kenya pamoja na viongozi kutoka Umoja wa Posta Afrika (PAPU) wakifuatilia mkutano wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) Bw. Sifundo Moyo na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe (hawapo pichani, katika ofisi za PAPU, jijini Arusha
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika ofisi za Shirika la Posta nchini mkoani Arusha, kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Shirika hilo mkoani humo
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe alipotembelea maendeleo ya ujenzi unaoendelea wa ofisi za Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ambapo Kenya ni nchi mwanachama wa Umoja huo, jijini Arusha
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya Bw. Daniel Kagwe alipotembelea Ofisi za Posta Kuu jijini Arusha