SHIRIKA LA POSTA LATEMBELEA MAHABUSU YA WATOTO
SHIRIKA LA POSTA LATEMBELEA MAHABUSU YA WATOTO.

Mkuu wa Kitengo cha Usalama kutoka Shirika la Posta Tanzania, Bi. Zuhura Pinde akizungumza wakati akikabidhi zawadi mbalimbali za Shirika hilo kwa Mahabusu ya watoto iliyoko Upanga, Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, Dar e's Salaam.
Katika kuelekea siku ya Wanawake Duniani, tarehe 7 machi 2022, baadhi ya Wafanyakazi Wanawake kutoka Shirika la Posta Makao Makuu, wametembelea na kutoa zawadi mbalimbali kwenye mahabusu ya watoto, Upanga Jijini Dar es Salaam.
Wanawake hao wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Usalama kutoka Makao Makuu ya Shirika la Posta, Bi. Zuhura Pinde wamekabidhi misaada hiyo kwa niaba ya Postamasta Mkuu, leo tarehe 7 Machi, 2020 kama mchango wa Shirika kwa jamii katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.
Naye Mkuu wa Mahabusu hiyo Bw. Darius Damas Kalijongo amelishukuru Shirika la Posta Tanzania kwa kukumbuka kutembelea Mahabusu hiyo ambapo amewapongeza wanawake hao kwa kujitoa kwao na kuwakumbuka watoto wanaolelewa katika Mahabusu hiyo.
"Kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, tunatoa pongezi sana kwa kina mama hawa wa Shirika la Posta Tanzania kwa kututembelea katika Mahabusu hii ya Watoto.
Niwatakie Kila la Kheri Katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani" alimalizia Bw. Darius.
Wanawake hao kutoka Makao Makuu ya Shirika la Posta walipata nafasi ya kuzungumza na watoto walioko kwenye mahabusu hiyo ambapo waliwahimiza watoto hao kuishi katika misingi ya maadili na nidhamu.
Imetolewa na:
Ofisi ya Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania
PICHA NA MAELEZO.

Baadhi ya wafanyakazi Wanawake kutoka Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, wakikabidhi zawadi mbalimbali kwa Mahabusu ya Watoto iliyoko Upanga, Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Mahabusu ya Watoto, Bw. Darius Damas Kalijongo akizungumza mara baada ya kupokea zawadi mbalimbali kutoka Shirika la Posta Makao Makuu, Jijini Dar es Salaam.

Afisa Mlezi Mahabusu ya Watoto Upanga, Bi. Daina Mwantabangale akizungumza mara baada ya kupokea zawadi mbalimbali kutoka Shirika la PostaTanzania.



