POSTA TANZANIA NA POSTA YA OMAN KUSHIRIKIANA KIBIASHARA.
POSTA TANZANIA NA POSTA OMAN KUSHIRIKIANA KIBIASHARA.
● NAPE AITAKA POSTA KUWEKA MKAZO KATIKA HUDUMA ZAKE ILI KUKIDHI MAHITAJI YA WANANCHI.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye amelitaka Shirka la Posta Tanzania kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Shirika ili kuhakikisha Shirika linakidhi na kutoa huduma stahiki kulingana na mahitaji ya Wananchi
Hayo ameyasema leo tarehe 31 Mei, 2022 wakati akishuhudia hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Oman, katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam
“Watendaji wa Shirika la Posta Tanzania wekeni mkazo katika utoaji wa huduma za Posta ili ziweze kukidhi mahitaji ya sasa ya wananchi na huduma hizo zisiwe na mashaka bali zenye ubora”. Amesema Mhe. Nape
Akizungumza na hadhara hiyo Waziri Nape ameeleza kuwa, ushirikiano kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Oman utaleta manufaa kwa Taifa kwani namna wananchi watakavyopata mwamko wa kutumia huduma za Posta ndivyo Serikali itaweza kupata mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi
Aidha, Mhe. Waziri ameongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaunga mkono juhudi zinazoendelea kufanywa na Shirika la Posta nchini katika kukuza mahusiano na mataifa mengine duniani na ametumia fursa hiyo kuzipongeza Posta hizo kwa kuona fursa katika ushirikiano kati ya Posta za mataifa haya mawili na kuwasisitiza kupanua wigo pale wanapoona kuna fursa
“Nawahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inaunga mkono juhudi hizi za pamoja mnazozifanya na iko tayari kushirikiana na ninyi ili kuhakikisha maono haya mliyonayo mnayatimiza kwa faida ya nchi hizi mbili”. Amesema Mhe. Nape
Katika hatua nyingine Mhe. Waziri Nape ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wageni kutoa nchini Oman kutembelea vivutio vilivyopo Tanzania ikiwemo mjini Zanzibar pamoja na mbuga mbalimbali zilizopo nchini ili waweze kujionea fahari ya nchi ya Tanzania, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais katika kutangaza utalii wa Tanzania.
Imetolewa na
Ofisi ya Mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Ndugu Macrice Mbodo akizungumza leo, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Oman, kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Oman, Ndugu Nasser Ahmed Al Sharji, akizungumza, katika hafla hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika(PAPU) Ndugu Sifundo Chief Moyo akizungumza, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Oman.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Posta Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Mabongo akizungumza, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Oman, kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam
PICHA ZA TUKIO HILO!!


















