SERIKALI KUSHUGHULIKIA MTAJI WA BILIONI 20.9 KWA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA.

SERIKALI KUSHUGHULIKIA MTAJI WA BILIONI 20.9 KWA SHIRIKA LA POSTA TANZANIA.

 606BBE54 241E 4A5F ABFA CAEE94FB608E

 Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto akizungumza wakati wa Kikao Kazi cha Viongozi wa Shirika la Posta kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo kikuu SUA, mjini Morogoro

 

 Na mwandishi wetu, Morogoro 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imeahidi kuendelea kushughulikia maombi ya mtaji wa Shirika la Posta Tanzania ili kuliwezesha Shirika kutekeleza majukumu yake kuendana na lengo la uanzishwaji wa Shirika kwa mujibu wa Sheria iliyounda Shirika hilo.

Hayo yameelezwa tarehe 03 Agosti, 2022 na Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto wakati akifungua Kikao Kazi cha Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu SUA, Mjini Morogoro.

Akizungumza wakati akifungua kikao hicho, Ndg. Mgonya ameeleza kuwa Serikali kwa kutambua mchango wa Shirika la Posta hasa katika Sekta ya Mawasiliano nchini inaendelea kushughulikia suala la kulipa Shirika hilo mtaji wa Bilioni 20.9, lengo likiwa ni kulitengenezea mazingira wezeshi Shirika la Posta katika kutimiza majukumu yake.

Aidha, Ndg. Mgonya ameongeza kuwa Ofisi yake kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewasilisha mapendekezo ya maombi ya mtaji wa Shilingi bilioni 20.9 kwa Wizara ya Fedha na Mipango na kuahidi kuendelea kufuatilia suala hilo kwa utekelezaji wa haraka ili kulifanya Shirika liendelee kutoa huduma stahiki na zinazoendana na mahitaji ya wakati ya wananchi.

“Nazifahamu changamoto mlizonazo ikiwemo maombi ya mtaji wa Shilingi bilioni 20.9, na niwahakikishie kupitia Mkutano huu, Ofisi ya Msajili wa Hazina kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari tumezibeba changamoto hizi, mbali na kuwasilisha maandiko haya Wizara ya Fedha na Mipango, tunaendelea na ufuatiliaji na tuna imani kuwa changamoto zote hizi zitafanyiwa kazi”. Amesema Ndg. Mgonya

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo ametumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kupitia ofisi ya Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto kwa kuendelea kulitengenezea Shirika mazingira wezeshi huku akielezea mipango ya Shirika katika kuendelea kuboresha huduma zake kupitia utekelezaji wa mpango mkakati wa 8 wa kibiashara wa Shirika kwa miaka minne (2022/23 - 2025/26) wenye dhumuni ya kuifanya Posta ya Kidijitali kwa biashara endelevu (Digitalization of Post for Business Improvement and Sustainability) lengo ikiwa ni kutoa huduma stahiki na zenye ubora kuendana na vionjo vya wateja

“Ili kuendana na vionjo vya wateja wetu vilivyobadilika na pamoja na kuendana na dira ya Taifa tumedhamiria kuifanya Posta ya Kidijitali kupitia mpango mkakati wetu wa 8 wa biashara wa Shirika ili kila mwananchi anufaike na huduma zetu”. Amesema Bw. Mbodo

Kikao hicho kilichowakutanisha viongozi wote wa Shirika la Posta kuanzia ngazi ya mikoa, Zanzibar na Makao Makuu kina lengo la kutathmini utendaji kazi wa Shirika kwa kipindi kilichopita cha mwaka wa fedha 2021/22 pamoja na kuangalia namna ya kutatua changamoto zilizojitokeza kwa kipindi cha mwaka huo uliopita na pia kusainiana malengo ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano;
Shirika la Posta Tanzania;
04 Agosti, 2022.

Picha zaidi za tukio hilo.

2DF95D24 0D70 4799 BA36 263E63559AC8

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania akizungumza wakati wa Kikao Kazi cha Viongozi wa Shirika hilo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo kikuu SUA, mjini Morogoro

0C3E9EA5 9446 4AB8 B921 3FD86E213236

 Meneja wa Posta mkoa wa Dodoma Bw. Ferdinand Kabyemela akitoa neno la shukrani mara baada ya ufunguzi rasmi wa Kikao Kazi cha Viongozi wa Shirika hilo, katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu SUA, mjini Morogoro

 8E3A7627 1A09 4846 9341 4F7E1BD92F92

Baadhi ya Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania wakifuatilia hotuba mbalimbali zilizokuwa zinatolewa wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha viongozi hao uliofanywa na Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto (hayupo pichani), katika ukumbi wa mikutano wa chuo kikuu SUA, mjini Morogoro 

BDDF89BD 4267 4B7A 9E4C 0F2B7DBE38EF 

Msajili wa Hazina Ndg. Mgonya Benedicto (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania mara baada ya kufungua rasmi kikao kazi cha Viongozi hao, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu SUA, mjini Morogoro

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Tanzania Census 2022

X

Tanzania Posts Corporation

You have no authorized to right click contents of TPC, All rights reserved!