JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

MBODO: “DKT. SAMIA APEWE MAUA YAKE”


 

Dar es Salaam

MBODO: “DKT. SAMIA APEWE MAUA YAKE”

Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Bw. Macrice Mbodo amewasilisha taarifa ya utendaji sambamba na mafanikio ya Shirika la Posta kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo katika taarifa hiyo ameeleza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kukuza Sekta ya Posta nchini

 

Ameeleza hayo tarehe 14 Agosti, 2023 wakati alipokuwa kwenye kikao na Wahariri wa Vyombo vya Habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

 

Bwana Mbodo alitumia mkutano huo kuelezea mafanikio yaliyopatikana ndani ya Shirika kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2022/23 iliwemo kuimarisha ulinzi na usalama wa mali za wateja kwa kuongeza mitambo mitatu ya kisasa ya ukaguzi wa mizigo pamoja na kuongeza Kamera za kisasa (CCTV Camera) 200, Utoaji wa huduma kidigitali ikiwemo Duka Mtandao la Posta na Huduma ya Posta Kiganjani.

 

Sambamba na hilo Shirika limeshiriki kufanikisha zoezi la sensa ya watu na makazi kwa kusafirisha na kusambaza vishikwambi na vifaa vingine vya sensa, Shirika limefanikiwa kusafirisha sampuli za kibaiolojia nchi nzima. Pia katika kuhakikisha Posta inakidhi  vionjo vya wateja, limeimarisha mtandao wa usafirishaji kwa kuongeza magari 14 kwa njia ya barabara.

 

Katika hatua nyingine Bwana Mbodo ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifungua Tanzania Kimataifa pamoja na kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Shirika.

 

“Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan apewe maua yake, amefungua mipaka ya nchi yetu hasa kwa sekta ya Posta tumepata nafasi ya kutambulika kimataifa”. Amesema Mbodo

 

Mbodo ameeleza kuwa, Shirika la Posta Tanzania limepata nafasi ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa mamlaka zote mbili za maamuzi ya Umoja wa Posta Duniani(UPU). Pia Shirika limefanikiwa kupewa fursa ya kuwa mwenyekiti mwenza na nchi ya Uswisi kuongoza kamati muhimu ya Baraza la Uendeshaji ya Huduma za Posta na Biashara Mtandao (Physical services and E commerce committee)

 

Postamasta Mkuu ameongeza kuwa Shirika kupitia utekelezaji wa mkakati wake wa 8 wa kibiashara (2022/2023 – 2025/2026) limedhamiria kuhakikisha kuwa Posta ya Tanzania inakuwa Posta ya mfano wa kuigwa na Posta zingine za barani Afrika. Vilevile kuwa Posta ambayo huduma zetu zote zitatolewa kupitia mfumo wa Posta Kiganjani pamoja na kuwa na Posta inayotoa huduma zote za Serikali mahala pamoja kama ilivyo sasa.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Bw. Deodatus Balile amelipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa juhudi mbalimbali inazozifanya katika kuboresha huduma zake hasa katika kipindi hiki cha maendeleo ya Sayansi na Teknolojia ili kuendelea  kufikisha huduma bora na stahiki kulingana na mahitaji ya wananchi

 

 

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano,

Shirika la Posta Tanzania,

14 Agosti, 2023

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA 2023