JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

SHIRIKA LA POSTA TANZANIA

Habari

TANZANIA YAONGOZA KIKAO UPU


TANZANIA YAONGOZA KIKAO CHA KAMATI NAMBA 2 YA BARAZA LA UENDESHAJI LA UMOJA WA POSTA DUNIANI (UPU)

Tanzania imeongoza kikao cha Kamati namba 2 ya Baraza la Uendeshaji la Umoja wa Posta Duniani (UPU) kwenye vikao vya Baraza hilo vinavyoendelea Jijini Berne, Makao Makuu ya Nchi, Uswizi.

Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti mwenza wa Kamati hiyo ya Huduma za Posta na Maendeleo ya Biashara Mtandao, Bwana Constantine Kasese akishirikiana na mwenzake kutoka Posta ya Uswizi Bwana Aime Theubert.

Kamati hiyo ni moja ya kamati nne za Baraza la Uendeshaji la Umoja huo. Kamati zingine ni Kamati namba 1 inayohusiana na Masuala ya Mnyororo wa Bidhaa na Huduma za Posta, Kamati namba 3 inayohusu Masuala ya Masoko na Ubunifu na Kamati namba 4 inahusika na Huduma za Fedha katika Mtandao wa Posta.

Ujumbe wa Tanzania kwenye vikao hivyo umeongozwa na Bi. Caroline Kanuti, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Posta kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Wengine ni Bw. Constantine Kasese, Mkurugenzi wa Biashara Mtandao na Huduma za Fedha na Bw. Elia Madulesi, Meneja wa Mahusiano na Mambo ya Posta Kimataifa, Shirika la Posta Tanzania pamoja na Bw. Muhinda Iddy kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa wote.

Vikao vya Baraza ya Uendeshaji na lile la Utawala la UPU yaliyoanza vikao vyake tarehe 30 Oktoba, 2023 yataendelea na vikao vyake hadi tarehe 10 Novemba, 2023 vitakapohitimishwa.

Tanzania ni Mjumbe wa Mabaraza yote Mawili ya Umoja huo yaani Baraza la Uendeshaji(Postal Operations Council) na Baraza la Utawala (Council of Administration).

Imetolewa na;

Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano

Shirika la Posta Tanzania,

31 Oktoba, 2023.

Rudi Juu

© SHIRIKA LA POSTA TANZANIA