Habari
MAADHIMISHO YA SIKU YA POSTA DUNIANI 2
MAADHIMISHO YA SIKU YA POSTA DUNIANI
Na mwandishi wetu,Dar es salaam
*Uzinduzi wa Stempu ya Pamoja na nchi
ya Oman
*Uzinduzi wa Stampy ya Tanzabia
inayohamasisha utalii wa ndani (Royal
Tour)
Tanzania kupitia Shirika la Posta kwa kushirikiana na Posta Oman imezindua Stempu ya Pamoja yenye lengo la kutunza na kuendeleza uhusiano wa kihistoria ulipo baina ya nchi hizi mbili. Pia Tanzania imezindua Stempu maalum yenye lengo la kuhamasisha utalii wa ndani (Royal Tour)
Stempu hizo zimezinduliwa rasmi na Mheshimiwa Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyofanyika Tarehe 9 Oktoba,2022 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na Naibu Balozi wa Oman Bwana Rashid Al-Manji aliyeongozana na Mtendaji Mkuu wa Posta ya Oman na Asyad Group Nasser Al Sharji pamoja na viongozi wengine kutoka Posta Oman na baadhi ya Viongozi kutoka nchini Tanzania.
Aidha, Stempu ya Pamoja na nchi ya Oman imetumia mchoro wa jengo la Maajabu maarufu kama "House of Wonders" lililopo Stone Town, Zanzibar, lengo ikiwa ni kutunza historia ya jengo hili ambalo lina mchango mkubwa kihistoria kati ya nchi hizi mbili.
Vilevile Stempu ya nchini Tanzania imetumia michoro ya wanyama wakubwa nchini yaani “Big Five” ikiwemo Simba, Tembo, Chui, Nyati na Faru, lengo ikiwa kuhamasisha utalii.
Ushirikiano wa Shirika la Posta Tanzania na Posta ya Oman ni muendelezo wa ushirikiano unaoendelea kutekelezwa na viongozi wa nchi hizi mbili.
Ikumbukwe kuwa Juni, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alitembelea nchi ya Oman pamoja na kuona namna ambavyo Posta ya nchini humo inafanya shughuli zake katika kuhudumia wananchi.
Ushirikiano huu ni endelevu na wenye tija katika kuhakikisha wananchi wananufaika na ushirikiano uliyopo, hususani katika huduma mbalimbali zinazotelewa katika nchi hizi hasa katika Sekta ya Posta.
Picha za matukio zaidi